Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeagiza biashara zote, yakiwamo maduka ilizofunga katika mikoa ya kusini Lindi na Mtwara, zifunguliwe na kuendelea kuhudumia jamii na Serikali iweze kupata kodi yake.
Aliyetangaza kusitishwa kwa uamuzi huo ni Kamishna wa kodi ya mapato za ndani, Elijah Mwandumbya, kwenye kikao cha pamoja kati yake na wafanyabiashara wa Mkoa wa Lindi.
Mwandumbya alitoa agizo hilo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wadau hao kwamba baadhi ya wafanyabiashara wakiwamo wa vifaa vya ujenzi, soda na vyakula katika mikoa hiyo, wamelazimika kuzifunga kwa madai kukadiliwa kodi kubwa tafauti na kile wanachokipata.
Kamishna huyo alisema uamuzi wa kufunga biashara sio jambo la busara, kwani licha ya kuwaathiri wafanyabiashara wenyewe, pia athari huigusa Serikali, kutokana na sehemu kubwa ya mapato yake kutokana na kodi zinazolipwa na wafanyabiashara.
“Sisi TRA ni wakala tu wa kukusanya maduhuri ya Serikali, leo mnapofunga mnategemea inapata wapi fedha za kutekeleza masuala ya maendeleo kwa jamii, ”alisema Mwandumbya.
Alisema Serikali inapokusanya kodi inaiwezesha kutekeleza kwa majukumu yake, ukiwamo ujenzi wa vituo vya kutolea huduma kwa jamii, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, miundombinu ya mawasiliano ya barabara, umeme na nyinginezo.
Aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaweka vizuri mahesabu yao, ili kuepuka usumbufu wa kukadiliwa kiwango kikubwa cha kodi tafauti na kile wanachokipata.
Baadhi ya wafanyabiashara, Obodea Swai, Said Namachokole, Ally Pepe, Selemani Ahamadi na Ally Bushiri walisema hivi sasa wafanyabiashara wengi wamelazimika kufunga shughuli zao kutokana na kiwango kikubwa cha kodi wanayokadiliwa.
Pia walimueleza Kamishna huyo kuwa hawakatai kulipa kodi kama sheria inavyowataka, lakini wanashindwa kutokana na mzunguko mdogo wa kifedha unaochangiwa na kukosekana kwa viwanda katika Mkoa wa Lindi.
“Tambueni watu mnaowaleta kuhudumu huku mnawapeleka mkoa masikini, hivyo msiwapangie viwango vikubwa vya ukusanyaji kodi,” alisema Namachokole.
Hatua hiyo ya TRA imechukuliwa siku chache baada ya Rais John Magufuli kutoa maelekezo ya kuangaliwa upya kodi wanazotozwa wafanyabiashara, kutokana na malalamiko mengi ya kukadiliwa kodi kubwa.
Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya pili ya reli ya kisasa kutoka Dodoma hadi Morogoro, Jumatato iliyopita, Rais alimwagiza Waziri wa Fedha na Mipango na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanaondoa kero za kodi ili kutoa hamasa kwa wananchi kulipa kodi kwa manufaa ya taifa.
Alisema ni vyema TRA ikaangalia kodi inazotoza kwa kuwa inawezekana zingine ni kubwa mno kuliko miradi ambayo wananchi wanatekeleza au kuwekeza.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, badala ya kuwa motisha kwa walipakodi, inakuwa kero kwa walipakodi, hivyo badala ya kulipa kodi wanabuni mbinu za kuwepa kodi wakati wangeelimishwa vizuri, wangeweza kulipa kodi.
0 Comments:
Chapisha Maoni