Mkurugenzi wa Mashtaka DPP amekata rufaa kupinga uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu, Firmin Matogoro wa kukataa hati ya kuzuia dhamana ya washtakiwa Antonia Zakaria na Timoth Kilumile wanaokabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 3/2018 walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza Januari 17 mwaka huu.
Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama na kujimilikisha mali Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU) na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh10 bilioni.
Baada ya kusomewa mashtaka, wakili wa upande wa mashtaka Seth Mkemwa anayesadiana na Shadrack Kimaro aliwasilisha hati ya kiapo ya DPP kuzuia dhamana kwa kile alichoeleza ni kulinda maslahi ya Taifa na usalama wa washtakiwa.
Baada ya kusikiliza hoja za upande wa utetezi unaowakilishwa na wakili Deocles Rutahindurwa, Jaji Matogoro uliitupilia mbali hati hiyo akisema haina uhalali mbele ya macho ya sheria kwa sababu imetoa hoja za jumla bila kueleza maslahi ya Taifa inayolindwa wala watakaowadhuru washtakiwa wakiachiwa kwa dhamana.
Katika uamuzi wake, Jaji Matogoro alikubaliana na upade wa utetezi kwa kusema DDP ametumia vibaya madaraka yake kuwasilisha hati hiyo kwa sababu kwa sababu anajua haiwezi kuhojiwa mahakamani ndio maana hakubainisha maslahi ya Taifa inayolindwa.
"Haiingii akilini namna gani usalama wa unavyotishiwa wala nani wanaoutishia wakati wameishi mitaani bila kudhurika tangu mwaka 2002 wanapodaiwa kutenda makosa hayo," alisema Jaji Matogoro katika uamuzi wake juzi.
Shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa leo Februari 27 baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa upelelezi umekamilika, lakini lilipoitwa ndipo wakili Shadrack alipoieleza mahakama kuwa DPP amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama wa kutupa hati ya kuzuia dhamana.
Jaji Matogoro ameahirisha shauri hilo hadi kesho Februari 28 rufaa hiyo ya DPP itakaposikilizwa.
0 Comments:
Chapisha Maoni