ZAIDI ya Shilingi Milioni 335 zimetumiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,unaomilikiwa na Kampuni ya madini ya Acacia,kukamilisha miradi miwili ya maendeleo katika kijiji cha Kakola,wilayani Kahama.
Akizungumza katika hafla ndogo ya makabidhiano ya miradi hiyo,Kaimu Meneja wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,uliopo kijiji cha Kakola katika Halmashauri ya Msalala,John Almot,alisema miradi hiyo imejengwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo wa Elimu.
Almot alisema Mgodi umekamilisha mradi wa maji katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo sambamba na kujenga uzio katika Shule za Msingi za Kakola A na B,ambazo ni changamoto za kipindi cha muda mrefu zilizokuwa zikilalamikiwa na wananchi.
Aliihakikishia jamii inayozunguka Mgodi kuendelea kutatuliwa changamoto zao mbalimbali,ambapo kwa kukamilisha mradi wa maji alisema utasaidia watu zaidi ya 30,000 katika Kata ya Kakola,kuondokana na tatizo sugu la uhaba wa maji huku uzio ukiwaweka wanafunzi katika mazingira salama ya kupata elimu.
Kwa upande wa jamii iliyopokea miradi hiyo ilipongeza kwa hatua hiyo,hususani kwa mradi wa maji safi na salama kwa kudai utasaidia kuondoa tatizo la uhaba mkubwa wa maji katika kata yao uliokuwa ukihatarisha afya zao kutokana na kutumia maji yasiyo salama.
“ Hivi ndivyo mwekezaji anatakiwa kuishi na jamii inayozunguka eneo lake la Uekezaji kutatua changamoto mbalimbali za jamii,tunashukuru sana kwani sasa hatutaathirika tena na magonjwa ya mara kwa mara ya tumbo,”alisema Lui Marko.
Aidha wanafunzi katika Shule hizo walidai kufarijika kwa miradi hiyo huku wakifurahia zaidi mradi wa maji ambao walidai umewaondolea adha kubwa ya kubeba vidumu vya maji kila siku asubuhi kutoka majumbani mwao.
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakola “A”,Joyce Lwanji,alisema kujengwa kwa uzio kwa ushirikiano na wadau wa elimu wilayani Kahama katika Shule hizo, kutasaidia kudhibiti vibaka na wavuta bangi waliokuwa wakiingia maeneo ya shule na kuharibu miundo mbinu mbalimbali.
“ Ukosefu wa uzio,ulisababisha mazingira yasiyo rafiki kwa walimu na wanafunzi,kwani ulisababisha hata nyakati za masomo watu kukatiza katikati ya shule na vijana wahuni kutumia vivuli vya miti kupumzika na kuvuta bangi mchana na usiku,”alisema Mwalimu Mkuu huyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala,Leonard Mabula,aliomba jamii ya Kata ya Kakola kuipa thamani miradi hiyo kwa kuitunza,kusudi wadau sambamba na Mwekezaji wa Mgodi wa Bulyanhulu,waone umuhimu wa kuchangia shughuli zingine za kijamii kwa mustakabari wa maendeleo ya kata na wilaya kwa ujumla.
0 Comments:
Chapisha Maoni