Rais Paul Kagame wa Rwanda leo amekuwa na mazungumzo mjini Paris na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, katika jitihada za kufungua ukurasa mpya katika Uhusiano wa nchi hizo mbili, uliozorota kwa karibu miaka 24.
Kuzorota huko kulitokana hatua ya dola hilo kubwa kuwaunga mkono waliofanya mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994. Mohammed Abdul-Rahman anawasimulia zaidi juu ya ziara hiyo.
Ni mara ya kwanza kwa rais Paul Kagame wa Rwanda kukutana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Ikulu ya Elyseee mjini Paris tokea 2011, wakati ambapo uhusiano wa nchi hizo mbili bado haujaimarika, ikiwa ni miaka 24 tokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994.
Rais kagame ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa Umoja wa Afrika, yuko mjini Paris ambapo kesho Alhamisi atahudhuria ukumbi wa kimataifa wa kiufundi unaojulikana kama VivaTECH.
Kabla ya hafla hiyo watakula chakula cha pamoja cha jioni na wakuu wa makampuni ya kiufundi wakiwemo Mkuu wa mtandao wa Facebook Mark Zuckerberg na Satya Nadella kutoka kampuni ya Microsoft. Rwanda inawania kuwa kituo kikuu cha masuala ya ufundi barani Afrika.
Kagame na Macron walishakutana mara mbili katika kipindi cha mwaka mmoja, kwanza wakati wa mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini NewYork na baadae nchini India katika mkutano kuhusu matumizi ya nishati ya Jua mjini New Delhi.
Pia Macron anapanga kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika , kama mgeni mualikwa, mkutano utakaofanyika Mauritania mwezi Julai.
0 Comments:
Chapisha Maoni