Mwenendo wa wasichana wa Kikristo wa jimbo la Kaduna nchini Nigeria kupendelea kuolewa na vijana wa Kiislamu, limepelekea kuibuka vurugu kubwa zilizoendana na umwagaji damu.
Takribani watu saba wameuawa na wengine 15 kujeruhiwa katika mapigano yaliyowahusisha wafuasi wa dini ya Ukristo kuwashambulia Waislamu jimboni hapo.
Habari zinasema kuwa, mapigano hayo ambayo yamejiri katika kijiji cha Kasuwa Magai eneo la Kajuru jimbo la Kaduna, yaliibuka baada ya wasichana kadhaa wa Kikristo kutaka kubadili dini na kuwa Waislamu ili waolewe na vijana wa Kiislamu, suala ambalo liliwafanya watu wa jamii yao kuchukizwa na suala hilo.
Katika tukio hilo vijana wa Kikristo walianzisha vurugu kubwa na mashambulizi kuwalenga Waislamu ambapo mbali na kuchoma moto nyumba kadhaa na maduka, yalipelekea pia watu saba kuuawa na wengine 15 kujeruhiwa.
Asilimia kubwa ya wakazi wa Kaduna ni Waislamu ambao licha ya vitendo vichafu vya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram, katika kuchafua sura halisi ya Uislamu ulioletwa na Mtume Muhammad (saw), wamekuwa wakiongezeka kila uchao kutokana na mafundisho yake ya kulingania upendo na amani kuwavutia wafuasi wa dini nyingine.
0 Comments:
Chapisha Maoni