MALUMBANO YAIBUKA UJENZI WA ZAHANATI ISAKA.
Malumbano yameibuka baina ya wakazi wanaoishi Kata ya Isaka,wilayani Kahama juu ya ukubwa wa eneo la ujenzi wa zahanati kwa baadhi wanaosadikiwa kuwa na maslahi nayo kutaka lipunguzwe na wengine wakitaka ukubwa ubaki kama awali.
Eneo hilo lilitengwa baada ya kupitishwa katika kikao cha baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Msalala,katika wilaya ya Kahama,limeingia katika marumbano makubwa juu ya ukubwa wa eneo lililotengwa kwa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Isaka Station,kwa baadhi kutaka lipunguzwe kisha kurejeshwa kwa wenye maeneo na wengine wakipinga uamuzi huo.
Hali hiyo ilijiri katika mkutano wa hadhara,ulioitishwa na Diwani wa Kata ya Isaka,Dk.Gerald Mwanzia, kwa lengo la kuondoa changamoto zinazokwamisha maendeleo katika kata hiyo .
Dk.Mwanzia alistaajabishwa na kitendo kilichofanywa katika mkutano mkuu wa kijiji cha Isaka Station,kilichofanyika Mei 31,mwaka jana,cha kupinga maamuzi ya baraza la madiwani lillotenga ukubwa hekari nane na kupitisha ramani ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.
Alisema kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala,kiliketi na kutoa maamuzi ya ukubwa wa eneo la ujenzi wa zahanati kwa kuangalia maslahi mapana ya siku za usoni kwa kutambua kuwa mji unakuwa kutokana na fursa za kiuchumi zilizopo eneo hilo.
Aidha alisema maamuzi yaliyopitiswa na Baraza la Madiwani yalistahili kuheshimiwa kwani ndio dira ya maendeleo ya kata hiyo,pindi kama waliona yanastahili kupingwa ungefuata utaratibu wa kisheria,kwa kufuata ngazi zinazohusika za mabaraza ya ardhi kuanzia ngazi ya vijiji,Kata hadi wilaya.
Akiongea kwa niaba ya waliopitisha azimio la kupunguza ukubwa wa ujenzi wa zahanati kutoka eneo la ukubwa wa heka nane hadi kuwa mraba wa mita mia,Richard Charles,alisema maamuzi ya mkutano wa Serikali ya kijiji yalitokana na kutambua kutomudu gharama za kulipa fidia kwa wenye maeneo.
Kwa upande wake Selemani Muya alikumbusha juu ya fursa ya kuwepo kwa Kituo kikubwa cha ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda kwenda Tanga,pia ujenzi wa reli ya kwenda Rwanda,na kuwaomba fursa hizo kuzitumia kwa kujiimarisha katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya na kuomba eneo lisipunguzwe kwa mustakabari huo.
Hata hivyo Diwani Dk.Mwanzia,alihitimisha mkutano huo kwa kuwasihi jitihada zifanyike za kutafuta wathamini ili itambulike thamani halisi ya fidia watakaostahili kulipwa watakaopisha ujenzi wa zahanati,kuliko kukimbilia kupunguza eneo pasipo kuangalia maslahi mapana baadaye kwa maendeleo ya ya mji wa Isaka.
0 Comments:
Chapisha Maoni