Mjumbe maalumu wa Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini amefanya safari nchini Korea Kaskazini ambapo pia amesema kuwa akiwa Pyongyang atajadiliana na viongozi wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya silaha za nyuklia.
Chong Yi-Yong ambaye atakuwa kwa siku mbili nchini Korea Kaskazini amesema kuwa atawasilisha suala la kuvuliwa silaha za nyuklia mbele ya viongozi wa nchi hiyo jirani. Ikiwa Yi-Yong atafanikiwa kukutana na Kim Jong-Un, Kiongozi wa Korea Kaskazini, basi huyo atakuwa kiongozi wa kwanza wa Korea Kusini kukutana na kiongozi huyo kijana tangu alipoingia madarakani na baada ya kufariki dunia baba yake mwishoni mwa mwaka 2011.
Aidha ikiwa Korea Kaskazini itakubaliana na suala la kuvuliwa silaha za nyuklia, basi huo utaweza kuwa mwanzo wa kuanza mazungumzo kati ya Pyongyang na Washington kwa ajili ya kuhitimisha mkwamo wa suala zima la silaha za nyuklia. Katika miezi ya hivi karibuni Korea Kusini na Korea Kaskazini zimekuwa na mahusiano mazuri tangu kulipojiri mazungumzo yaliyoishawishi Pyongyang kutuma wanamichezo wake kwa ajili ya kushiriki michuano ya msimu wa baridi iliyomalizika hivi karibuni.
Mgogoro kati ya Marekani na Korea Kaskazini ulishika kasi baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump wa Marekani na baada ya rais huyo kutoa vitisho dhidi ya taifa hilo. Hii ni kwa kuwa kwa mara kadhaa Trump alitishia kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo, suala lililoifanya Pyongyang kujibu vitisho hivyo dhidi yake.
AWASILI SALAMA.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un anaandaa mkutano wa chakula cha jioni na wajumbe wawili kutoka Korea Kusini, ikiwa ndiyo mara ya kwanza kiongozi huyo anakutana na ujumbe kutoka Kusini tangu aingie madarakani mwaka 2011.
Shirika la habari la Korea Kusini la Yonhap, liliripoti kuhusu mkutano huo likimnukuu msemaji wa rais nchini Korea Kusini.
Ujumbe huo uko nchini Korea Kaskazini kwa mazungumzo yasiyo ya kawaida yenye lenngo la kuanzisha mchakato kati ya Korea Kaskazini na Marekani.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeboreka kufuata mashindano ya olimpiki ya msimu wa baridi.
Ujumbe huo unawajumuisha maafisa wenye vyeo vya mawaziri - mkuu wa ujasusi Suh Hoon na mshauri wa usalama wa taifa Chung Eui-yong.
Awali Bw Chung aliwaambia waandishi wa habari kuwa atawasilisha azimio la Rais Moon Jae-in la kudumisha mazungumzo na kuboresha uhusiano kati ya Korea Kaskazini na Kusini na kuondoa silaha za nyuklia kutoka Rasi wa Korea.
0 Comments:
Chapisha Maoni