MWITO umetolewa kwa wadau wa afya mkoani Shinyanga,kufanya jitihada za kufanikisha tiba ya magonjwa mbalimbali yanayowakabili watoto wenye ulemavu mchanganyiko wanaolelewa katika kituo cha Buhangija Jumuishi,mjini Shinyanga.
Mwito huo ulitolewa na Kaimu Mkuu wa Kituo cha Buhangija Jumuishi,Mwalimu Mohamed Makana,wakati wa kukamilisha shughuli za
uchunguzi na utoaji tiba kwa magonjwa ya Kinywa na Meno,uliofanywa na jopo la madaktari bingwa wa Chama cha madaktari wa Kinywa na Meno Tanzania ( TDA ).
Mwl. Makana alisema mbali na matibabu ya maradhi hayo ya Kinywa na Meno kufanywa na Madaktari bingwa kutoka TDA kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kusaidia kupunguza magonjwa hayo,lakini kituo hicho bado kinakabiliwa na maradhi mengine.
Alibainisha kuwa watoto katika kituo hicho hususani Albino wanakabiliwa na magonjwa ya ngozi na macho,hivyo ni vyema wadau mbalimbali wa afya wakajitokeza kusaidia kutatua changamoto za maradhi hayo ili kuwanusuru vijana hao,ambao ni tegemeo kwa uzalishaji mali na maendeleo ya taifa hili kwa kipindi kijacho.
Kiongozi wa jopo la Madaktari hao,Dkt. Anorld Mtenga,alisema kwa kipindi hiki katika kituo hicho hali ya Afya ya Kinywa na Meno imezidi
kuimarika na idadi ya watoto wagonjwa wanaobainika imepunguatofauti na kipindi cha mwaka 2014 walipofikwa kwa mara ya kwanza katika kituo hicho.
Alisema wamefanyia uchunguzi watoto 225 katika kituo hicho na kati yao 51 ndio waliowabaini kuwa na matatizo tofauti ya maradhi ya Kinywa na Meno na kuwapatia matibabu yanayowastahiki idadi ambayo ni ndogo kulingana na mazingira wanayoishi.
Aidha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Rashid Mfaume,aliiasa jamii ya mkoa wa Shinyanga kuwaelekeza watoto wao jinsi ya kufanya usafi wa Kinywa na Meno kwa ufasaha tangu wangali wadogo,hatua itakayosaidia kupata kinga sahihi hivyo kukabiliana na maradhi hayo.
Alifafanua kwa kutambua suala hilo la kukabiliana na maradhi hayo katika kipindi hiki cha kuelekea kilele cha siku ya kinywa na meno
Duniani kitakachofanyika Kitaifa katika wilaya ya Tarime,mkoani Mara,mkoa kupitia maafisa wake kutoka idara ya afya wanaendelea kutoa
elimu kupitia wadau mbalimbali wa afya.
Na Ally Lityawi, Kahama.
0 Comments:
Chapisha Maoni