KAULI YA UN YACHOCHEA MOTO SYLIA, NI BAADA YA KUSEMA MASHAMBULIZI YASITISHWE.

Serikali ya Syria imefanya mashambulizi makubwa ya anga na ardhini katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi Ghouta Mashariki, siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa haraka mapigano.

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake Uingereza, limesema kuwa kiasi ya watu 13 wanaoviunga mkono vikosi vya serikali na wapiganaji sita wa kundi la waasi wa Jaish al-Islam, wameuawa katika mashambulizi yaliyofanywa leo.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Rami Abdel Rahman amesema mapigano yanafanyika katika eneo la Al-Marj ambalo ni eneo la mapambano linalodhibitiwa na waasi karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus.
Zaidi ya raia 500 wauawa tangu kuanza mapigano.
Ameongeza kusema kuwa mashambulizi ya leo ni mabaya zaidi kufanyika tangu utawala wa Syria ulipoanzisha operesheni mwezi huu wa Februari. Zaidi ya raia 500 wameuawa katika operesheni hiyo iliyoanzishwa wiki iliyopita Mashariki mwa Ghouta.
Mashambulizi hayo yanafanyika siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura kwa kauli moja kutaka kusitishwa mapigano nchini Syria kwa siku 30 na kuruhusu kupelekwa misaada ya kibinaadamu na kuwaondoa raia kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kwa upande wake kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ametoa wito wa kusitishwa haraka mapigano nchini Syria na kuruhusu kupelekwa misaada ya kiutu, hasa kwenye eneo linalodhibitiwa na waasi, Ghouta Mashariki ambalo limekuwa likishambuliwa na vikosi vya serikali.

Hayo yanajiri wakati ambapo Urusi imesema kuwa inavitegemea vikosi vya kigeni vinavyoipinga serikali ya Syria kuhakikisha mapigano yanasitishwa kama ilivyopendekezwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana. 

Taarifa iliyoandikwa katika tovuti ya wizara ya mambo ya Urusi imeeleza kuwa nchi hiyo imeyataka makundi hayo kusitisha mapigano ili kuruhusu kupelekwa misaada ya kibinaadamu.
Akizungumza leo wakati akiwabariki waumini, Papa Francis amesema katika miaka saba ya machafuko nchini Syria, mwezi huu wa Februari umekuwa wenye machafuko zaidi na huo ni ukatili. Ameongeza kusema kwa mtu hawezi kupambana na uovu kwa kutumia uovu mwingine.
Hata hivyo, Iran imesema itaendelea na mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi karibu na Damascus, kwa sababu azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa vita Ghouta Mashariki halikuyalenga makundi ya kigaidi.
Share on Google Plus

About huhesofm blog

0 Comments:

Chapisha Maoni