Huduma za tohara kwa wanaume zimeshamiri mkoani Shinyanga ambapo zaidi ya wanaume 47,500 wamenufaika na huduma hiyo katika kipindi cha Mwezi Oktoba 2016 hadi Machi 2017 kupitia kampeni ya Tohara Kinga ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili kujikinga na maambukizi ya VVU.
Kampeni hiyo inaendeshwa na serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Intrahealth International kwa ufadhili wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Maambukizi ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia Centre for Diseases prevention and Control (CDC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana,Mratibu wa kudhibiti maambukizi ya VVU mkoa wa Shinyanga Dkt. Mawazo Amri Saleh amesema serikali imekuwa ikishirikiana na shirika la Intrahealth International katika kuendesha huduma ya tohara kwa vijana na wanaume kuanzia miaka 10 na kuendelea.
Alisema tangu waanze kampeni hiyo katika halmashauri sita za mkoa wa Shinyanga mwezi Oktoba 2016 mpaka mwezi Machi 2017, zaidi ya wanaume 47,500 wamepatiwa huduma ya tohara bila malipo yoyote.
Alisema huduma hizo zilitolewa kupitia mfumo wa huduma vituoni na huduma za nje ya vituo zinazotolewa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali zipatazo 50 katika wilaya zote za mkoa wa Shinyanga.
“Lengo la kampeni hii ni kuwapatia huduma wanaume 95,900 katika kipindi cha mwezi Oktoba 2016 hadi Septemba 2017 lakini mpaka sasa tumefikia asilimia 50 ya lengo lililokusudiwa”, alieleza Dkt. Saleh.
Alizitaja faida za tohara kwa wanaume kuwa ni pamoja na kujikinga na maambukizi ya VVU kwa asilimia 60,kuwa msafi,kujikinga na magonjwa ya ngono,kujikinga na kansa ya kichwa cha uume na kuwakinga akina mama kansa ya mlango wa kizazi.
Aliongeza kuwa zoezi la tohara kwa wanaume linazidi kuwa na mwitikio mzuri kwani wanaume wengi wamekuwa wakijitokeza kupata huduma ya tohara.
“Tunatoa shukrani kwa shirika la IntraHealth kwa ushirikiano mzuri wanaoutoa katika utoaji huduma za tohara mkoani hapa,tunaamini kuwa kutokana na mipango IntraHealth tuliyopanga kwa mkoa na wilaya lengo la mkoa la kufikia asilimia 80 ya tohara kwa wanaume wote mkoani hapa litafanikiwa”,aliongeza Dkt. Saleh.
Naye Mshauri wa Kiufundi wa masuala ya tohara mkoa wa Shinyanga kutoka shirika la Intrahealth International, Dkt. Innocent Mbughi alisema mbali na mkoa wa Shinyanga hivi sasa shirika hilo linatekeleza pia mradi wa tohara ya mwanaume katika mikoa ya Mwanza, Geita, na Simiyu ambapo katika kipindi cha mwezi Novemba 2016 hadi Machi 2017, zaidi ya wanaume 127,000 wamepatiwa huduma za tohara.
Dkt. Mbughi alisema wamefikia asilimia 50 kwani lengo ni kuwapatia huduma za tohara wanaume wapatao 256, 529 katika kipindi cha mwezi Oktoba 2016 hadi Septemba 2017 katika mikoa hiyo ambapo pia huduma ya upimaji wa hiari wa VVU inatolewa.
Dkt. Mbughi alibainisha kuwa shirika la Intrahealth International kwa ufadhili wa Mfuko wa rais wa Marekani wa Kupambana na Maambukizi ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia Centre for Diseases prevention and Control (CDC) limekuwa likishirikiana na serikali kupitia wizara ya afya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, kitengo cha kuzuia kuenea kwa maambukizi ya VVU (NACP), kamati za afya za mkoa na wilaya na wadau wengine wa afya katika kutoa huduma bora za tohara kwa wanaume.
Serikali ya Tanzania imeandaa mpango wa kitaifa wa kutekeleza huduma za tohara ili kufikia lengo la kitaifa la asilimia 80 kutoka asilimia 72 kwa sasa (THIMS report 2011) ambapo kipaumbele kimeelekezwa kwenye mikoa yenye viwango vya chini vya huduma za tohara na maambukizi ya VVU.
Mikoa hiyo ni Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Katavi, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, Ruvuma na Mara wilaya ya Rorya.
0 Comments:
Chapisha Maoni